MAPISHI



257 Votes

 MAPISHI YA MWAMBAO VYAKULA VIKUU
BSHHH

WALI WA ASUMINI

Mchele kilo 1
Kuku mkubwa 1
Vitunguu maji kilo 2
Mayai 8
Samli kilo 1
Thomu gram 200
Tangawizi mbichi gram 50
Mdalasini gram 50
Hiliki gram 50
Bizari nzima kiasi
Siki kiasi
Mtindi painti 1
Tungule kilo 1
Zabibu nyeusi kiasi
1                    Mkate kuku umwoshe umchemshe kwa maji na chumvi mpaka awive, kisha muepue.
2                    Menya vitunguu uvioshe uvikate na uvigawe sehemu mbili. Sehemu moja uiweke, sehemu ya pili vikaange mpaka viwe vyekundu kama vya biriani. Kisha vichuje uitoe samli yote, vitie katika sinia uvitandaze ili vipoe kwa kupata upepo.
3                    Chukua mdalasini, hiliki na bizari utwange pamoja, kisha uchunge unga laini. Saga thomu na tangawizi mbichi. Saga tungule.
4                    Teleka sufuria tia samli ile ile iliyokaangiwa vitunguu halafu utie vile vitunguu vilivyobakia uvikaange. Vikianza kuiva tia viungo ulivyovitwanga na kuvisaga. (Bakisha vitunguu na viungo kidogo). Tia vipande vya kuku, mtindi  siki na supu ya kuku iliyobakia katika sufuria. Acha ichemke nyama pamoja na vitu vyote  mpaka libaki rojorojo.
5                    Teleka maji, yakichemka tia chele. Ukiiva utoe uchuje yatoke maji yote.
6                    Teleka tena sufuria utie samli kidogo utie na vile vitunguu ulivyovibakisha uvikaange. Tia mdalasini nzima, kaanga pamoja, tia na ule wali ukoroge koroge ili uchanganyike na viungo. Kisha ufunike upalie moto.
7                    Chemsha mayai yote uyamenye.
8                    Wali ukishakauka utaupakua, lakini lazima itabidi utumie kombe au sahani kubwa itakayoweza kuingia wali pamoja na vitu vyote. Kuupakua kwake kwanza utatia nusu ya wali katika hiyo sahani, baadae utatia masalo na nyama yote, na mayai, kisha utayafunika masalo kwa wali uliobakia. Mwisho utachukua vile vitunguu ulivyovikaanga na ukavitandaza ili vipo, utavimwaga juu ya wali.Kwani ni kwa sababu ya hivi vitunguu ndio maana ukaitwa wali wa asumini. Ukipenda utapamba chembe za zabibu juu yake. ZABIBU HIZO Ziroweke kwanza ili zivimbe.

WALI WA BIRIANI

Mchele kilo 1
Nyama kilo 1
Samli ½ kilo 
Mbatata ½ kilo 
Vitunguu maji kilo 1
Thomu gram 150
Tangawizi mbichi gram 150
Hiliki gram 50
Mdalasini gram 100
Mtindi painti 1
Siki kiasi
Majani ya nanaa fungu moja
Chumvi kiasi
Zaafarani kidogo (irowekwe kwa maji ya moto nusu kikombe cha kahawa)
Tungule ilosagwa
Tungule ya kopo
1                    Menya vitunguu maji uvioshe uvikate. teleka sufuria utie samli, ikichemka tia vitunguu uvikaange bila ya kuvivuruga mpaka viwe vyekundu. Vichuje uvitoe halafu vitandaze katika sinia.
2                    Twanga mdalasini na hiliki mpaka viwe laini kama unga. Menya thomu uitwange pamoja na tangawizi mbichi.
3                    Kata nyama vipande vikubwa kisha tia chumvi na vitu ulivyovisaga (yaani tangawizi mbichi na thomu) vile vile tia unga unga wa mdalasini na hiliki pamoja na mtindi wa maji. Pika mpaka karibu nyama kuiva kabisa ndipo utie mbatata. Ukiona mbatata zimeshaiva tia siki.Usiache kukauka kabisa, bakiza rojorojo. Tia maji katika sufuria na chumvi yakichemka tia mchele. Acha utokote, angalia kiini cha wali ukiona umeshaiva uchuje.
4                    Angalia sufuria ya nyama na rojo lake lisiwe limekauka kabisa, lazima ziwe na maji kidogo. Chukua vile vitunguu ulivyovikaanga vikapoa uvinyunyuzie juu ya masalo yote (usikoroge). Halafu utie mchele uliouchuja, nyunyuzia maji ya zaafarani juu ya wali wote halafu unyunyuzie samli ile uliyochuja kutoka kwenye vitunguu ulivyovikaanga ienee juu ya wali wote. Kisha funika upalie makaa.
5                    Wali ukishakuwa tayari utaupakua. lakini unapotaka kuupakua lazima kwanza uutoe wali wote mweupe uutie katika chombo chengine, halafu uyakoroge masalo yachanganyike sawasawa kisha ndio uyatie juu ya wali katika kila sahani.

BIRIANI YA SAMAKI

Mchele kilo 1
Samaki kilo 1
Vitunguu kilo 1
Samli ¾ kilo
Thomu kiasi
Mdalasini kiasi
Hiliki kiasi
Ndimu kiasi
Tungule kiasi
Chumvi kiasi
1                    Mkate kate samaki umtie chumvi na ndimu umkaange. menya vitunguu uvikate. saga tungule, thomu na viungo vyote vilivyobakia. (Bakisha mdalasini nzima kidogo).
2                    Teleka sufuria utie samli, ikichemka tia vitunguu uvikaange, vikianza kupiga wekundu tia tungule na viungo kidogo. Acha vikaangike kwa muda mdogo halafu tia vipande vya samaki, chumvi na ndimu, pamoja na maji kidogo. Acha ichemke kwa muda mdogo. Likibaki rojorojo epua.
3                    Chukua sufuria jengine uitie maji na chumvi. yakichemka osha mchele utie. acha utokote. Angalia kiini cha wali, ukiona umeshaiva umimine uyachuje maji yote. Teleka tena sufuria utie samli kidogo, ikichemka tia vitunguu kidogo pamoja na vile vilivyobakia.Vyote vikaange kidogo halafu umimine wali wote ukoroge koroge ili upate kuchanganyika na viungo. Halafu uweke vizuri upalie moto. Ukishakauka utaupakua. Kuupakua kwake kwanza utatia wali kwenye sahani, baadae ndio utatia samaki pamoja na rojo rojo lake lote kwa juu.

WALI WA PILAU

Mchele kilo 1
Nyama kilo 1
Samli ¼ kilo
Vitunguu maji ½ kilo
Vitunguu thomu gram 100
Tangawizi mbichi gram 100
Mdalasini gram 50
Hiliki gram 25
Pilipili manga gram 100
Zabibu gram 100
Chumvi kiasi
1                    Teleka nyama utie chumvi na maji uipike mpaka iive. Baadae epua uiweke (ubakishe supu itakayotosha kuweza kuivisha mchele).
2                    Menya vitunguu uvikate. Menya vitunguu thomu na tangawizi mbichi utwange pamoja. Menya hiliki uitwange pamoja na bizari nzima. osha vijiti vya mdalasini pamoja na chembe za pilipilimanga uziweke. Osha zabibu uziweke. Menya mbatata uzioshe uziweke.
3                    Teleka sufuria tia samli, ikichemka tia vitunguu uvikaange. Tia thomu na tangawizi mbichi uliyoisaga tia vipande vyote vya nyama bila supu, tia mbatata na viungo vyote ulivyovisaga na kuviosha, isipokuwa zabibu. Kaanga kwa muda mfupi, baadae tia supu yote. Ikianza kuchemka tia mchele, onja chumvi. Angalia kiini cha mchele, ukiona wali umeiva na kukauka, fukua kati utie zabibu zote na baadae funika upalie moto.

PILAU YA PAPA MKAVU

Mchele kilo 1
Papa mkavu kilo 1
Vitunguu ½ kilo
Samli ¼ kilo
Bizari nzima kiasi
Thomu kiasi
Mdalasini kiasi
Hiliki kiasi
Chumvi kiasi
1                    Mkatekate papa umuoshe umchemshe, halafu umuoshe tena atoke mchanga wote, kisha mueke.  Kata vitunguu, saga thomu, hiliki na bizari nzima.
2                    Teleka sufuria utie samli, ikichemka tia vitunguu uvikaange. Vikianza kupiga wekundu tia thomu pamoja na viungo vyote vilivyobakia ukaange kidogo kisha tia maji na chumvi. Acha yachemke kisha tia mchele. Acha uchemke mpaka yakauke maji yote. Fukua kati umtie papa wote halafu upalie moto.
3                    Wali ukishakauka utaupakua kwa upole bila ya kumvuruga papa.

WALI WA CHOOKO

Mchele kilo1
Chooko ½ kilo
Samli kiasi
Nazi 2 nzuri
Vitunguu thomu kiasi
Bizari nzima kiasi
Vitunguu maji kiasi
Hiliki kiasi
Mdalasini kiasi
Chumvi kiasi
Karafuu chembe 2 au 3
1                    Osha mchele pamoja na chooko uweke pembeni.
2                    Kuna nazi uchuje tui kama la wali wa nazi uliweke.
3                    Menya vitunguu maji, uvioshe uvikate uviweke. Menya vitunguu thomu uvitwange pamoja na bizari na hiliki. Osha vijti vya mdalasini na chembe za karafuu uziweke.
4                    Teleka sufuria utie samli, ikichemka tia vitunguu uvikaange. Baadae tia viungo vyote ulivyovitwanga utie na chembe za karafuu pamoja na vijiti vya mdalasini. Kisha tia tui la nazi. Likianza kufumba tia mchele pamoja na chooko zake utie na chumvi. Acha utokote mpaka wali ukauke. Ukishakauka funika upalie moto.

BIRIANI YA KUKU

Mchele kilo 1
Kuku mkubwa 1
Samli ½ kilo
Mbatata ½ kilo
Vitunguu maji kilo 1
Thomu gram 150
Tangawizi mbichi gram 150
Hiliki gram 50
Mdalasini gram 100
Mtindi painti 1
Siki kiasi
Chumvi kiasi
Zaafarani kiasi (iroweke katika maji ya moto nusu kikombe cha kahawa)
1                    Meya vitunguu maji uvioshe uvikate. teleka sufuria utie samli, ikichemka tia vitunguu uvikaange mpaka viwe vyekundu. Vichuje utoe samli yote kisha vitandaze vipate kupoa.
2                    Twanga mdalasini na hiliki viwe laini, menya thomu na tangawizi utwange pamoja.
3                    Mkatekate kuku umtie chumvi, mtindi, thomu, tangawizi, na unga wa hiliki na mdalasini, na umpike.(Akiwa mgumu sana tia maji kidogo). Kisha tia siki umpike mpaka aive na abaki rojo rojo. Chemsha mbatata mbali kisha uzitie.
4                    Teleka sufuria nyengine utie maji na chumvi, yakichemka tia mchele. Angalia kiini cha wali, ukiona umeshaiva umimine katika chujiouchuje maji yote.
5                    Angalia sufuria yenye kuku isiwe imekauka, lazima iwe na rojo rojo. Iweke tena juu ya moto, uchukue vile vitunguu ulivyovitandaza vipoe uvinyunyizie  vyote juu ya masalo ya kuku. Kisha utie wali wote juu yake. Chukua maji ya zaafarani utie kwa juu na utie samli yote uliyoichuja kwenye vitunguu. Kisha funika upalie moto. Wali ukishakauka utaupakua kwenye sahani kisha utamweka kuku na masalo yote juu yake. 

PILAU YA KUKU

Mchele kilo 1
Kuku mkubwa 1
Samli ¼ kilo
Vitunguu ½ kilo
Thomu gram 100
Tangawizi mbichi gram 100
Mdalasini gram 50
Hiliki gram 50
Bizari nzima gram 25
Zabibu gram 100
Pilipili manga kiasi
Chumvi kiasi
1                    Mkate kuku umpike kwa maji na chumvi mpaka aive. wakati wa kumuepua angalia kuwa ana supu itakayotosha kuivisha mchele.
2                    Menya vitunguu uvioshe na kuvikata pamoja. Menya thomu na tangawizi mbichi pamoja. Twanga bizari nzima na hiliki. Osha vijiti vya mdalasini na chembe za pilipili manga uweke kando.
3                    Teleka sufuria utie samli, ikichemka tia vitunguu uvikaange. Vikianza kupiga wekundu tia thomu na tangawizi mbichi pamoja na viungo vyote vilivyobakia. Kaanga kidogo kisha tia mbatata na vipande vya kuku na umimine supu yote. Ikianza kuchemka tia mchele. Acha utokote. Onja chumvi.Angalia, ukiona wali umeshakauka fukua kati utie zabibu kisha palia moto.Wali ukishakauka utaupakua. kama unavyopakua wali wa pilau na nyama.
BOKOBOKO
Ngano nzima kilo 1
Nyama kilo 2
Mchele ¼ kilo
Samli ½ kilo
Vitunguu kiasi
Thomu kiasi
Bizari nzima kiasi
Hiliki kiasi
Mdalasini kiasi
Giligilani kiasi
1                    Teleka ngano na nyama na maji upike mpaka viive viwe laini sana. Osha mchele utie. Saga vitunguu pamoja na viungo vyote uvitie na uendelee kuvipika vyote pamoja huku unavikoroga mpaka vichanganyike na viive vyote na maji yote yakauke. (Unaweza kutia chumvi kidogo ukipenda). Funika upalie moto.
2                    Utakapokauka funua uanze kulisonga bokoboko. Lisonge mpaka lishikane sawasawa halafu liipue.
3                    Chukua samli uichemshe pamoja na hiliki kisha kila unapopakua utakuwa unalilazalaza na kulitengeneza kwa samli. Wengine hupenda kutengeneza kishimo kati kati yake na kukijaza samli ya moto. Watu wengine hupenda kulila tupu,  na wengine hula kwa sukari au kwa mchuzi wake ambapo hutengenezwa mahsusi.


MCHUZI WA BOKO BOKO

Tende au zabibu kilo1
Samli ¼ kilo
Vitunguu kiasi
Thomu kiasi
Giligilani kiasi
Bizari nzima kiasi
Siki kiasi
Hiliki kiasi
Sukari kiasi
1                    Ziroweke zabibu ndani ya maji kisha uzifikiche mpaka zilainike (usizikamue ukayatoa masimbi yake). Kama ni tende, zitoe kokwa uzikande na kuzivuruga kwa maji. menya vitunguu uvikate. Menya thomu usage pamoja na viungo vyote.
2                    Teleka sufuria utie samli, ikichemka tia vitunguu uvikaange. Vikianza kupiga wekundu tia viungo vyote, ukaange. Kisha tia zabibu au tende na sukari na siki. Ikiwa maji uliyorowekea tende ni kidogo, ongeza mengine kidogo. Acha ichemke kisaha epua.
NDIZI MBIVU
Ndizi mbivu za kupika 10
Nazi kavu 3
Sukari kiasi
Hiliki kiasi
1                    Zipasue ndizi katikati kwa marefu, uzitoe moyo wake.
2                    Zimenye kisha maganda uyaoshe. Yapange vizuri maganda hayo ndani ya sufuria safi (kwa chini). Chukua vipande vya ndizi uvipange juu ya maganda.(ndizi ziweke chali, usizifudikize).
3                    Kuna nazi uchuje tui zito mbali na jepesi mbali. Chukua tui jepesi ulitie katika ndizi kisha uziteleke. Zipike mpaka tui likauke na ndizi ziive. Nyunyuzia sukari kidogo. Twanga hiliki utie juu yake. Chukua lile tui zito ulimimine uache liwe linatokota kwa moto mdogo sana. Tui likikauka na kutoa mafuta epua na uziache zipoe. Unapopakua, zitoe taratibu bila ya kuzivuruga.

NDIZI MBICHI
Ndizi 15 au 20
Nazi kavu 2
Vitunguu kiasi
Thomu kiasi
Ndimu kiasi
1                    Zimenye ndizi uzipare na utoe utomvu wote. Zikate vipande vipande. teleka sufuria utie maji ya kiasi cha kuivisha ndizi.
2                    Kuna nazi uchuje tui zito mbali na jepesi mbali. Menya vitunguu uvikate. saga thomu.
3                    Maji yakikauka tia vitunguu, chumvi na thomu pamoja na tui jepesi. Acha litokote mpaka tui lote jepesi likauke. Mwisho tia ndimu kidogo ukipenda, utie na tui zito. Acha zitokote mpaka karibu na kukauka ndipo uepue.
TAMBI ZA NAZI
Tambi kilo 1
Sukari ¼ kilo
Nazi kavu 2
Hiliki kiasi
Arki kiasi
1                    Teleka maji, yakichemka zitie tambi zichemke kidogo, kisha zimimine katikachujio au kumto yatoke maji yote.
2                    Kuna nazi uchuje tui zito. Menya hiliki utwange utie katika tui.
3                    Liteleke tui ulipike na huku unalikoroga, kisha tia tambi utie na sukari uwe unazigeuzageuza kwa mwiko mpaka tui lote likauke lianze kutoa mafuta.
4                    Ziepue uache zipoe. baadae zipakue.
TAMBI ZA KUKAANGA
Tambi kilo 1
Sukari ¼ kilo
Samli ¼ kilo
Hiliki kiasi
Arki kiasi
Zabibu (zioshe uziroweke kidogo kwenye maji ya moto).
1                    Zichukue tambi uzivunjevunje katika sinia au ungo.
2                    Teleka sufuria juu ya moto utie samli. Ikichemka tia tambi zote uwe unazikaanga mpaka zipige wekundu. Tia sukari, hiliki au arki pamoja na maji ya moto. Acha zichemke mpaka uone kiini cha tambi kisiwe laini sana na maji yote yakauke.
3                    Ziepue uache zipoe kidogo. Baadae zimimine kwenye sahani. chukua zabibu upambie juu yake.
VIPOPOO VYA UWANGA
Uwanga ½ kilo
Sukari kilo 1
Nazi 6
Hiliki kiasi
Arki kiasi
1                    Uchunge uwanga uwe safi sana. Kuna nazi uchuje tui zito mbali na jepesi mbali. Menya hiliki uitwange.
2                    Ukande uwanga kwa maji ya moto uufinyange donge. Katakata madonge madogo madogo halafu uyasokote. Baadae ukate vipopoo vidogo vidogo, kama chembe za mbaazi au hata vidogo kuliko hivyo.
3                    Teleka sufuria utie maji, yakichemka vitie hivyo vipopoo vyote uache vichemke kidogo halafu vimimine kwa haraka katika chujio yatoke maji yote.
4                    Teleka tena sufuria utie tui jepesi, sukari, arki na hiliki upike na huku unakoroga. Tui likianza kuchemka, vitie vipopoo vyote uwe unavikoroga mpaka viwe vimeshakauka vizito vya kiasi viepue. Kupakua kwake tafuta sahani ndogo ndogo za shimo au vibakuli vidogo vidogo uvitie na baadae uviweke kwenye upepo vipate kuganda.
 MAPISHI YA MWAMBAO  VITOEO
HHH

KUKU WA KUPAKA

Kuku mkubwa 1
Nazi nzuri 2
Tungule kubwa 2
Vitunguu kiasi
Limau kiasi
Chumvi kiasi
Vitunguu thomu kiasi
Hiliki kiasi
1                      Mteleke kuku ndani ya sufuria yenye nafasi bila ya kumkata. Mtie chumvi, limau na maji kidogo umpike mpaka akaukie na aive.
2                      Menya vitunguu uvisage. Menya vitunguu thomu na hiliki usage pamoja. Menya tungule uzisage.
3                      Kuna nazi uchuje tui zito kisha uvitie vitu vyote ulivyovisaga ndani ya tui. Lipike na huku unalikoroga mpaka liwe zito na lishikane.
4                      Mchukue kuku umtumbukize ndani ya tui uwe unamgeuza geuza mpaka tui likauke lianze kutoa mafuta.
5                      Toa moto wote ubakie vuguvugu, kisha mfunike umpalie makaa kidogo. Baada ya muda mfupi mfunue umtie kwenye sahani, kisha utoe tui lote lililobaki kwenye sufuria ulipake juu ya kuku.

KUKU WA KUIKIZA

Kuku mkubwa 1 
Vitunguu kilo 1
Samli kilo 1
Tungule kilo 1
Mayai 8

Maoni